Meneja wa Manchester City Pep Guardiola amesema kuwa anaiheshimu sana Crystal Palace inayohaha katika kampeni za Ligi Kuu Uingereza kuelekea mechi yao katika uwanja wa Etihad Jumamosi.
Eagles wamekuwa na mwanzo mbaya msimu huu katika historia yao kwenye Ligi Kuu, wakiwa wamepoteza mechi tano za mwanzo bila kufunga hata goli moja.
Kocha wa zamani wa Uingereza Roy Hodgson alichukua mikoba ya Frank de Boer kama meneja wa Palace wiki iliyopita lakini alishindwa kuleta mabadiliko ya haraka timu hiyo ikiambulia tena kipigo cha 1-0 dhidi ya Southampton katika Selhurst Park.
City wapo kileleni mwa msimamo wa ligi na wameshinda mechi zao tatu za mwisho katika michuano yote kwa jumla ya magoli 15-0, lakini Guardiola amesisitiza kuwa ushindi dhidi ya timu ya Hodgson si jambo la uhakika.
"Naheshimu sana kile nilichokiona kutokakwa Palace dhidi ya Southampton na Burnley," aliwaambia wanahabari Ijumaa mchana. "Wametengeneza nafasi nyingi. Niliwaonyesha wachezaji wangu nafasi zote walizotengeneza, katika mechi mbili tu. Wataingiza mipira mingi mirefu ndani ya boksi na krosi.
"Namkubali Roy Hodgson, amekuwa akishughulika na soka muda mrefu na anastahili kupewa heshima yake. Napenda nguvu alizo nazo na ni mzoefu na soka la Ulaya."
Safari ya Palace kwenda City ni mwanzo wa ratiba ngumu ambayo mbele yake watakutana na Manchester United na Chelsea.

No comments:
Post a Comment