Yanga imezidi kujikongoja kutetea ubingwa wake baada ya leo kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Majimaji ya Songea
Mshambuliaji wakimataifa wa Zimbabwe Donald Ngoma, leo ameinusuru timu yake ya Yanga na kipigo kutoka kwa Majimaji baada ya kuifungia bao la kusawazisha dakika ya 79 akiunganisha krosi iliyopigwa na Mzambia Obrey Chirwa katika pambano la Ligi ya Tanzania Bara lililopigwa uwanja wa Majimaji Songea.
Hiyo ni mara ya pili kwa Ngoma kuinusuru Yanga kwa kipigo msimu huu, mara ya kwanza ilikuwa kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Lipuli FC, uliochezwa uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, lakini yeye aliisawazishia timu hiyo dakika tatu kabla timu hizo hazijaenda mapumziko.
Majimaji ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza lililofungwa na Peter Mapunda dakika ya 54, kufuatia pasi nzuri ya kiungo Abdulihalim Humud.
Sare hiyo inaifanya Yanga kufikisha pointi 5 wakati Majimaji wanafikisha pointi mbili hivyo kuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha wanapambana na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufanya vizuri kwenye ligi ya msimu huu.
Katika mchezo huo wenyeji Majimaji waliuanza mchezo kwa kasi na kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la Yanga lakini mabeki wa Yanga walikuwa imara na kuondosha hatari zote langoni mwao.
Yanga ilizinduka na kuanza kupanga mashambulizi yake vizuri lakini ubovu wa uwanja ilikuwa kikwazo kwa timu zote hasa Yanga ambao wamezoea kucheza kwenye uwanja wa Uhuru au ule wa Taifa Dar es Salaam, ambavyo vinanyasi halisi na kingine bandia.
Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa sare ya bila kufungana huku umiliki wa mpira ukiwa 50-50, lakini Yanga walitengeneza nafasi nyingi za kufunga kuliko wenyeji wao Majimaji ambao walikuwa akicheza kwa kujihami huku wakitumia mashambulizi ya kustukiza.
Kipindi cha pili kocha wa Majimaji Habibu Kondo, aliwaingia wachezaji wakongwe Jeryson Tegete na Abdulihalim Humud, ambao walionekana kuongeza nguvu na kasi ya mashambulizi kwenye lango la Yanga.
Katika dakika ya 48 ya mchezo mshambuliaji Ibrahim Ajibu wa Yanga alipoteza nafasi ya wazi kuifungia timu yake bao la kusawazisha baada ya kushindwa kumalizia krosi iliyochongwa na Geofrey Mwashiuya na kipa Endrew Ntala alifanya kazi nzuri ya kupangua mpira huo.
Baada ya kuingia kwa bao hilo Yanga walizinduka na kuzidi kupambana kwa kumiliki mpira lakini Majimaji walikuwa makini kwenye kujilinda na kuondosha hatari langoni mwao.
Pamoja na kufanya mashambulizi mengi bila kupata bao kocha George Lwandamina aliamua kumtoa Juma Abduli na kumuingiza Hassani Kessy ambaye alisaidia kupandisha mashambulizi mbele na kupiga krosi nyingi langoni mwao.
Jitihada za Yanga ziliweza kuzaa matunda dakika ya 79, ambapo Ngoma aliunganisha kwa kichwa mpira uliopigwa na Chirwa na kusawazisha bao hilo ambalo lilikuwa likisubiriwa kwa hamu na mashabiki wao ambao muda wote wa mchezo alikuwa kimya.
Kuingia kwa bao hilo kuliwaongezea kasi ya mashambulizi Yanga na kuliandama lango la Majimaji, lakini wapinzani wao alicheza kwa umakini huku wakitumia mbinu ya kujiangusha kupoteza muda ili kupata ushindi.
Katika dakika ya 85, mchezaji wa Yanga Emmanuel Martin alilazimika kutolewa nje, baada ya kupoteza fahamu kufuatia kugongana na mchezaji wa Majimaji, lakini baadaye madaktari wa timu hiyo walimpa huduma ya kwanza na kurudi kwenye hali yake ya kawaida.
Yanga imemaliza mechi za kanda ya Kusini kwa kupata pointi nne, baada ya ushindi wa bao 1-0, walioupata Jumamosi iliyopita dhidi ya Njombe Mji ya Njombe na Jumamosi ijayo watakuwa nyumbani uwanja wa Uhuru kucheza na Ndanda FC ya Mtwara.